Mlima Kilimanjaro wazua mzozo mafunzoni Marekani
Na Jacqueline Liana, Milwaukee, Winsconsin
MLIMA Kilimanjaro umesababisha mzozo miongoni mwa Watanzania na Wakenya wanaoshiriki mafunzo ya utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa, mjini hapa.
Tukio hilo lilitokea juzi Septemba mwaka huu, wakati wakiwa darasani katika Chuo Kikuu cha Marquette, mjini hapa, chanzo kikiwa ni Dk. Thomas Bausch, raia wa Marekani, aliposema ni katika miaka ya karibuni amefahamu mlima huo uko Tanzania na si Kenya.
“Wamarekani wengi ndivyo wanavyojua, nilishangaa sana,” alisema Dk. Bausch na kuongeza kuwa Watanzania wanatakiwa kuutangaza Mlima Kilimanjaro ujulikane uko kwao.
Kauli hiyo iliwafanya baadhi ya Watanzania wanaohudhuria mafunzo hayo ya wiki sita kujibu kwa msisitizo, kwamba Mlima Kilimanjaro uko Tanzania, huku wakimwambia Dk. Bausch, ‘karibu Tanzania upande Mlima Kilimanjaro’.
Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela ndiye aliyeongoza ‘mashambulizi’ kwa upande wa Watanzania, kwa kumwambia Dk. Bausch ambaye ni mtu mzima wa makamo kuwa, yeye ni mmoja wa wabunge katika mkoa wa Kilimanjaro na ndiko mlima ulipo.
Baadhi ya Wakenya walikuwa wakiingilia kati wakati Anne alipokuwa akimweleza Dk. Bausch kwa kusema ‘hata ukiwa Kenya unauona Mlima Kilimanjaro.’
Anne aliwataka wanyamaze na kuwaambia kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakieneza uongo huo.
“Huo ni uongo wa kimataifa, Mlima Kilimanjaro uko Tanzania,” alisisitiza Anne na kuongeza “Katika masuala ya msingi yanayohusu nchi yangu sitaki mchezo.”
Anne alitoa mfano kwamba, kama mtu ana nyumba yake, na jirani yake anaiona, je jirani huyo anaweza kutangaza ni yake kwa sababu anaiona akiwa kwake?. Dk. Bausch akajibu hapana.
Mfanyakazi wa Wizara ya Afya ya Kenya, Sylivia Shitsama, alitoa doa zaidi pale alipohoji, kama hiyo nyumba ina manufaa na haitumiwi, kuna ubaya gani kwa mtu mwingine kuitumia. Kauli hiyo ilifuatiwa na mguno wa nguvu kutoka kwa Watanzania, wakiashiria kutokubaliana naye.
Katika hatua nyingine, Dk. Bausch ambaye aliwahi kuwa mshauri wa wanafunzi katika chuo kikuu hicho kwa miaka zaidi ya 10, alisema aliwahi kuzitembelea Tanzania na Kenya. Alisifu Kenya wana chai nzuri, na Anne alimjibu kwamba siku nyingine akirudi Tanzania asikose kuulizia chai ya Njombe kwani nayo ni ‘bomba’.
Watanzania wengine wanaohudhuria mafunzo hayo, ni Naibu Spika Anne Makinda, Mbunge Injinia Mohamed Mnyaa na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Caesar Waitara.
Wengine ni Hakimu Mkazi Batista Mhelela kutoka mkoa wa Ruvuma, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya afya mkoani Kilimanjaro, Veronica Shao, Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi na Nyumba mkoa wa Ilala, Dar es Salaam, Lusungu Hongoli na mfanyakazi wa Bunge, Anselm Mrema.
000
Mlima Kilimanjaro ni salama kupandwa’
‘NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema mlima Kilimanjaro ni salama kupandwa na si hatari kama ilivyoelezwa na vyombo vya habari vya kimataifa.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Blandina Nyoni, ilisema kuwa, hakuna vifo vya watalii wanaokufa ovyo wanapopanda mlima huo.
Ilisema, takwimu sahihi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na ofisi ya Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, zinaonyesha idadi ya wapagazi waliokufa kati ya mwaka 2000 na 2007 ni sita, na kwamba vifo vyao vilikuwa vya kawaida.
“TANAPA inahakikisha kuwa kampuni zote zinazoratibu safari za watalii kupanda mlima Kilimanjaro, zinatimiza vigezo vya usalama kabla ya kuruhusu kundi au mtu mmoja mmoja kupanda mlima huo, “ iliongeza taarifa hiyo.
Mlima Kilimanjaro hupandwa na takribani watalii 40,000 kila mwaka, ambapo mapato yake huingia katika pato la taifa litokanalo na sekta hiyo.
“Taarifa iliyochapishwa siyo sahihi, kilichoelezwa siyo kile kilichotokea katika uendeshaji wa biashara ya utalii katika mlima Kilimanjaro, “ ilisisitiza taarifa hiyo, na kuwataka waandishi waliotoa habari hizo kujitokeza ili kuzirekebisha.
Gazeti la Times Online la Mei 26 na The East African la Juni 2, mwaka huu, yalidai kuwa, wapagazi na waongoza watalii 20 hufariki kila mwaka, na kwamba idadi ya vifo vya watalii ni mara mbili ya hivyo.
Kuondoka Mbeki ni pigo kwa Afrika -JK
Na Maura Mwingira, New York- Marekani
MWENYEKITI wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, amesema kuondoka madarakani kwa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ni tukio la kusikitisha na pigo kwa bara la Afrika.
Rais Kikwete alisema Mbeki ni mmoja wa viongozi wa aina yake, aliyejitolea kusimamia kwa dhati kuhakikisha Afrika inasonga mbele kiuchumi.
Alitoa msimamo huo juzi, alipozungumza na klabu ya waandishi wa habari wa kimataifa, wanaofanya kazi makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini hapa.
Kauli ya Rais Kikwete ilitokana na swali aliloulizwa na mmoja wa waandishi hao, kwenye mkutano uliomhusisha pia Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Donald Kaberuka.
“Niseme tu kwamba hili ni tukio la kusikitisha, ni pigo kwa Afrika. Tumempoteza kiongozi mashuhuri na madhubuti, aliyesimama kidete kuhakikisha Afrika inasonga mbele kiuchumi,” alisema Rais Kikwete.
Mbeki alipangiwa kuwa Mwenyekiti mwenza na Rais wa Bosnia na Herzegovina, Haris Silajdzic, kuendesha mjadala kuhusu changamoto za maendeleo barani Afrika na athari zake katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.
“Wote tunafahamu na ni mashahidi wa namna Mbeki alivyoasisi na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano Mpya wa Maendeleo Afrika (NEPAD),” alifafanua Rais Kikwete.
Viongozi wakuu wa nchi na serikali wapo mjini New York, kuhudhuria mkutano wa 63 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Ulitanguliwa na mkutano, ambao viongozi kutoka mataifa ya Afrika, taasisi za fedha na nchi wahisani walijadili namna ya kuogeza kasi ya kusaidia na kusukuma maendeleo ya Afrika.
Rais Kikwete alisema Mbeki pia aliasisi uamsho na uhuishwaji wa ujenzi mpya wa bara la Afrika, uliojielekeza katika ufufuaji wa uchumi, uwezo wa kujenga na kusimamia demokrasia na kutokomeza ukoloni mamboleo kati ya Afrika na mataifa makubwa.
Alisema alikuwa mstari wa mbele na alishiriki kikamilifu katika juhudi za upatanishi na upatikanaji wa amani na demokrasia ya kweli barani Afrika.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amesema hataraji kwamba, kuyumba kwa soko la hisa na mitaji la Marekani, kunaweza kukawafanya nchi wahisani kushindwa kutekeleza ahadi zao kwa bara la Afrika.
Alisema wakati nchi wahisani na tajiri zilipoahidi kuongeza kiwango cha misaada yao ya maendeleo kwa Afrika, haikuwa imetarajiwa wala kutegemewa kwamba, uchumi wa Marekani ungeyumba.
Soma Majina ya dawa, changamoto zake kwa watumiaji na wasimamizi wa huduma za matibabu
Suala la dawa ni muhimu katika huduma za matibabu. Ipo dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya Watanzania kwamba mtu akienda hospitali asipopata dawa au sindano na badala yake akapata ushauri, mtu huyo huwa anajihesabu kama hakutibiwa.
Jina asilia dhidi ya jina la kibiashara (Brand vs Generic) Majina ya dawa na mahali dawa hiyo ilipotengenezwa vimekuwa vikileta changamoto kubwa kwa watumiaji na katika suala zima la tiba hasa kwenye vipengele vya ubora wa dawa husika, uwezo wake wa kutibu na usalama wa dawa hiyo kwa mtumiaji.
Kwa sasa tutaangalia changamoto moja ya majina ya dawa. Hapa ninalenga tofauti iliyopo kati ya jina asilia la dawa (Generic name) na jina la kibiashara la dawa (Brand/Trade name).
Jina asilia la dawa ni nini? Kwanza ningependa kuwafahamisha kwamba kila dawa inayotengenezwa kitaalamu inakuwa na majina matatu kama ifuatavyo: Kwanza jina la kikemikali mfano: Acetaminofen, pili, jina la asilia mfano Paracetamol na tatu, jina la kibiashara mfano Panadol, Sheladol, Tulizamol na mengineyo.
Majina haya yote hapo juu ni majina ya dawa moja paracetamol ambayo wengi wameizoea kwa jina la kibiashara la mtengenezaji mvumbuzi au jina lenye hati miliki (Brand name) yaani Panadol.
Hivyo basi jina asilia la dawa ni lile jina lililokubalika kutumika kimataifa ambapo ukilitaja jina hilo mahali popote duniani mtu anaelewa unazungumzia dawa gani (International Non Propietary Name INN) kwa kufuata mfano wetu hapo juu ni Paracetamol.
Jina la kibiashara la dawa (Brand/Trade name) ni nini? Hili ni jina ambalo kampuni inayotengeneza dawa inaamua kuipa dawa husika. Dawa moja inaweza kuwa inatengenezwa na kampuni nyingi tofauti na kila kampuni ikachagua jina lake ambalo wataona watumiaji watalitambua haraka na kuamua kununua dawa yao badala ya kampuni nyingine.
Mfano Paracetamol inaitwa Calpol, Sheladol, Tulizamol au Cetamol. Hata hivyo, pamoja na dawa kuwa na majina tofauti ya kibiashara kuna jina la kibiashara ambalo dawa hupewa na mtengenezaji wa kwanza wa dawa hiyo mwenyewe.
Mara nyingi dawa hizi za mtengenezaji wa kwanza (mwenye hati miliki) huwa ni ghali sana kwani mtengenezaji anakuwa ametumia muda na fedha nyingi katika utafiti na utengenezaji wa dawa husika, hivyo mtengenezaji huyo hutaka kurudisha gharama alizotumia pamoja na kupata faida wakati watengenezaji wanaofuata hutumia kazi za mtengenezaji wa kwanza kupata faida.
Kwa nini hatimiliki katika dawa? Kwa kawaida dawa huchukua muda wa miaka minane hadi 12 tangu kuvumbuliwa mpaka ianze kuuzwa.Muda huu ni mrefu sana na fedha nyingi huwa zimetumika hivyo mtengenezaji wa dawa kwa mara ya kwanza hupewa muda wa miaka mitano kuuza dawa yake pekee kabla watengenezaji wengine hawajaruhusiwa kuitengeneza ili aweze kurudisha gharama zake.
Na kwa kitaalamu ‘brand medicine’ ni dawa, hizi zinatoka kwa mvumbuzi wa dawa hiyo yaani mmiliki wa hataza (patent owner) na wengine wote wanaofuata kutengeneza dawa hiyo zinaitwa kitaalamu ‘generic medicines’.
Hata hivyo, watu wengi wamekuwa na mazoea ya kuita dawa zote zilizotengenezwa viwanda vilivyoko Ulaya na Marekani ndio ‘Brand Product’ na zile zilizotengenezwa India na nchi za Afrika ndio ‘generic’.
Lakini kitaalamu dawa zinazoitwa ‘brand product’ ni zile zilizotengenezwa na mtengenezaji au mvumbuzi wa dawa wa awali yaani mtengenezaji mwenye hatimiliki.Tofauti kubwa iliyopo kati ya dawa generic na dawa brand kutoka kwa mvumbuzi ni bei kwani dawa ya mvumbuzi huwa ghali sana.
Tofauti nyingine ni katika majina ya kibiashara na viambatanisho vingine vinavyotumika katika kutengeneza dawa husika.Nchi zote zenye mamlaka za kudhibiti dawa haziruhusu utengenezaji au uingizaji wa dawa hizi asilia bila ya kufanyia majaribio ya kutosha kuhakiki kuwa dawa hizi zitakuwa na ubora, uwezo wa kutibu na usalama kwa mtumiaji kama dawa ile iliyotengenezwa na mvumbuzi wa dawa husika (bioequivalence testing).
Hata hivyo kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ambapo asilimia 80 ya dawa zote katika soko zinaagizwa kutoka nje ya nchi, udhibiti wa ubora wa dawa zote katika soko ni mgumu na hivyo kukuta kiasi kikubwa cha dawa bandia (counterfeit) na dawa zisizo na ubora (substandard) ni kubwa katika soko.
Kwa nini orodha ya dawa ya MTBA inatumia majina asilia ya dawa?
Sera ya Taifa ya Dawa inasisitiza uwezeshaji wa upatikanaji wa dawa muhimu kwa wote na matumizi sahihi ya dawa.
Hivyo basi ili kuwezesha upatikanaji wa dawa kwa watu serikali kwa kufuata miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inasisitiza matumizi ya dawa asilia, kwani dawa ambazo zina hatimiliki ni za ghali sana hivyo matumizi ya dawa asilia huongeza uwezo wa kununua dawa nyingi zaidi na hivyo kuongeza upatikanaji kwa watu wengi zaidi.
Ili kuhakikisha kuwa dawa hizi asilia (generic) zinakidhi viwango vya ubora, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) ili kuhakikisha kuwa suala hili linasimamiwa vizuri na kitaalamu.
Kama tulivyoona hapo mwanzo kwamba jina asilia la dawa ndilo jina linalotambulika kote duniani, hivyo waganga na wafamasia wanafundishwa dawa kwa kutumia majina asilia na si majina ya kibiashara. Kutokana na miongozo hiyo na Sera ya Taifa ndio maana orodha ya dawa ya MTBA inatumia majina asilia na si vinginevyo.
Vilevile MTBA imesajili vituo vya kutolea tiba vile tu ambavyo vimesajiliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ili kumhakikishia mfaidika wa Mfuko anapata huduma bora kwa gharama zinazokubalika, hii ikiwa ni pamoja na kupata dawa asilia zenye ubora.
Mfuko unaamini vituo hivi vinatunza dawa ambazo ubora, uwezo wa kutibu na usalama wake vimehakikiwa TFDA. Hata hivyo, pale ambapo dawa inayopatikana ni ile yenye hatimiliki pekee, basi Mfuko hulipia wanachama wake. Mfano Cellcept kwa wagonjwa waliobadilishiwa figo au ilivyokua kwa Coartem katika tiba ya malaria.
Kwa kumalizia ningependa kuwafahamisha mambo mawili muhimu. Kitaalam brand product ni ile dawa iliyotolewa na mtengenezaji wa kwanza yenye hatimiliki pekee. Watengenezaji wengine wanaofuata dawa hizo huitwa generic products hata kama imetengenezwa na viwanda vikubwa vya Ulaya na Marekani.
Ningependa mfahamu kwamba bei ya dawa inategemea na gharama za uzalishaji ndio maana dawa zilizotengenezwa Ulaya na Marekani ni ghali kuliko dawa zilizotengenezwa Asia na Afrika hii imepelekea watu wengi kufikiria kwamba dawa zote za Ulaya na Marekani ni brand product na zile za Asia na Afrika ndizo generic pekee, kumbe sivyo. Kama jambo hili lilikuwa linakutatiza natumaini umepata mwanga wa kutosha.
000000000
wapendwa ndugu zangu hasa wana blog napenda kuwafahamusha kuwa mimi noor shija mwandishi wa magazeti ya uhuru, mzalendo na burudani nimeamua kuingia kilingeni kushirikiana na nanyi katika kuhabarisha watu kupitia blog.
pia napenda kuwaletea tanzia ya mwandishi mwenzangu katika magazeti ya uhuru marehemu Ramadhan Kinyonya.
Imehaririwa: 24.09.2008 0101 EAT
Gazeti: Uhuru
•
Mwandishi Uhuru afariki dunia
KALALE SALAMA KINYONYA
Na Mwandishi WetuMWANDISHI wa habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Ltd (UPL), inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Ramadhan Kinyonya amefariki dunia.Kinyonya (40), alifariki dunia jana saa 7.00 mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu tangu wiki iliyopita.Alifikishwa hospitali hapo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa homa ya mapafu.Kinyonya alijiunga na UPL mwaka jana. Aliwahi kufanya kazi katika magazeti ya Mtanzania, Majira, Mwananchi na Kampuni ya Global Publishers, inayochapisha magazeti ya Uwazi na Champion.Hadi mauti yalipomfika, Kinyonya alikuwa mwajiriwa wa UPL, akiwa mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Uhuru.Kwa waliomfahamu Kinyonya wakati wa uhai wake, alikuwa mchapakazi hodari, mcheshi na mtu wa utani, aliyependa kutaniana na wenzake katika mambo mbalimbali.Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na ndugu wa marehemu. Taarifa zaidi kuhusu wapi na lini atazikwa zinatarajiwa kutolewa leo.Kinyonya alizaliwa mwaka 1968 mkoani Shinyanga. Alisoma katika shule za msingi na sekondari mkoani humo hadi mwaka 1987.Baadaye alijiunga na mafunzo ya cheti cha uandishi wa habari, elimu ya kompyuta na upigaji wa picha.
Thursday, September 25, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment