Wednesday, October 29, 2008
Ban Ki-moon awaasa waandishi wa habari
Na Maura Mwingira,New York-Marekani
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, ametoa wito kwa waandishi wa habari duniani kote, kuandika habari zinazowahusu watu wanyonge, masikini na wasio kuwa na sauti, licha ya mazingira magumu na vikwazo mbalimbali wanavyokumbana navyo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema UN inatambua mazingira magumu wanayofanyia kazi waandishi wa habari, na amewataka kutokata tamaa.
Mbali na hilo alisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa daima utapinga na kukemea vitendo vyovyote vinavyolenga kuathiri utendaji kazi wao.
Katibu Mkuu alitoa wito huo wakati wa chakula maalumu kilichoandaliwa kwa heshima ya waandishi wa habari wanne, ambao wamefadhiliwa na taasisi ya Dag Hammarskjold, kuja Umoja wa Mataifa, kujifunza na kuandika habari za umoja huo.
Miongoni mwa waandishi hao ni Erick Kabendera kutoka Tanzania anayeandikia gazeti la The Citizen. Kabendera anakuwa mwandishi wa tatu kutoka Tanzania kupata ufadhili wa taasisi hiyo, ikiwa ni miaka zaidi ya 20 tangu mwandishi wa mwisho kutoka Tanzania kufanikiwa kupata ufadhili wa taasisi hiyo.
Mwandishi Mwandamizi wa Magazeti ya Serikali (Daily News) Mkumbwa Ali, ni mmoja wa waandishi waliowahi kufanikiwa kupata ufadhili wa taasisi hiyo.
Jumla wa waandishi wa habari 200 walishindania nafasi nne ambapo, Erick Kabendera (Tanzania), Patricia Caycho (Peru),Grevazio Zulu(Zambia) na Ebtihal Mubarak (Saudi Arabia) kazi zao ziliwaridhisha majaji na kuteuliwa kuja Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi hiyo ya Dag Hammarskjold.
Ban Ki-moon alisema katika mazingira ya sasa ambapo dunia imekumbwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo za kuyumba kwa uchumi wa dunia, ni rahisi kwa wananchi wanyonge na masikini kusahaulika.
Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa pia na mabalozi kutoka mataifa mbalimbali, Ban Ki-moon alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari, na kuishukuru taasisi ya Dag Hammarskjold kwa kazi nzuri ya kutoa nafasi kwa waandishi kujifunza utendaji kazi wa kila siku wa Umoja wa Mataifa.
Akisoma taarifa yake iliyowasisimua na kuwagusa wageni waalikwa katika hafla hiyo, Kabendera, alielezea changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania hususan katika nyanja za huduma za afya na elimu.
Kabendera aliieleza hadhara hiyo, kwamba pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuboresha huduma za afya ili kinamama wajawazito wajifungue katika mazingira yaliyo salama na bora, bado uwezo wa serikali ni mdogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment