Thursday, September 25, 2008

• Kinyonya kuzikwa Shinyanga kesho

• Kinyonya kuzikwa Shinyanga kesho


Na Mwandishi Wetu

MAZISHI ya mwandishi wa habari wa Kampuni ya Uhuru Publications Ltd (UPL), inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Ramadhan Kinyonya, yanatarajiwa kufanyika kesho mkoani Shinyanga.
Taarifa iliyotolewa na familia ya marehemu jana ilisema mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kesho asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Precision kwenda Shinyanga na mazishi yamepangwa kufanyika jioni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa leo saa 7.00 mchana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Kinyonya (40), alifariki dunia juzi saa 7.00 mchana katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu tangu wiki iliyopita.
Alifikishwa hospitalini hapo kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa homa ya mapafu.
Kinyonya alijiunga na UPL mwaka jana baada ya kufanyakazi katika magazeti ya Mtanzania, Majira, Mwananchi na Champion.
Hadi mauti yalipomfika, Kinyonya alikuwa mwajiriwa wa UPL, akiwa mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Uhuru.
Kinyonya alizaliwa mwaka 1968 mkoani Shinyanga. Alisoma shule za msingi na sekondari mkoani humo hadi mwaka 1987 alipomaliza kidato cha nne.
Baadaye alijiunga na mafunzo ya upigajipicha, uandishi wa habari na kompyuta ngazi ya cheti.


00000000000

No comments: