Saturday, September 27, 2008

mambo ya wakubwa

Mmetonaaaaaa wajemeniiii!!!!!!!!




Mama wa shoka Condeleezza Rice akiwa kwenye tizi hakuna mchezooooo!





Hapo safi mama




Zoezi la baiskeli lina raha yake



Kuoga ni muhimu sana



Nadhani hii habari ina ukweli!



Unasema...?



00000000000000000


UN yataka serikali za mitaa ziwezeshwe

Na Maura Mwingira, New York- Marekani

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, amesisitiza wajibu wa serikali za mitaa katika kufanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia (MDG).

Alisema wajibu huo unatokana na ukweli kwamba, chombo hicho ndicho kilicho karibu zaidi na wananchi, ambao ndio walengwa wa MDG.

Dk. Asha- Rose alisema bila ya juhudi za makusudi zitakazozishirikisha serikali za mitaa kuanzia ngazi ya kata, kijiji, wilaya, miji na mikoa, mafaniko yaliyokwisha kupatikana yanaweza kurudi nyuma.

Naibu Katibu Mkuu huyo alikuwa akifungua mjadala kuhusu wajibu na ushiriki wa serikali za mitaa katika utekelezaji wa MDG, ulioandaliwa na serikali ya Italia na kufanyika makoa makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mijadala kadhaa ilifanyika jana kuhusu malengo ya milenia, ikifunguliwa na Dk. Asha-Rose; Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Baraza Kuu la 63 la Umoja wa Mataifa, Miguel D’Escoto.

Ahadi ya dola za Marekani bilioni 16 ilitolewa na makundi mbalimbali ya kijamii, zikiwamo taasisi za fedha, wafanyabiashara, nchi wahisani na watu maarufu katika mijadala hiyo.

Dola za Marekani bilioni 1.6 zimetolewa kwa ajili ya usalama wa chakula, dola bilioni 4.5 kwa mpango wa kuendeleza elimu na zingine kwa ajili ya kupamba na malaria.

Kwa mujibu wa Dk. Asha-Rose, ili serikali za mitaa ziweze kutekeleza majukumu yake vizuri, ni muhimu kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika kuziwezesha.

“Serikali za mitaa ndizo zinazotoa dira na mwelekeo wa maisha ya wananchi… zinaendesha vituo vya afya na zahanati, shule na kutoa hudumu muhimu kama za majisafi na majitaka.

“Ni lazima tuzisaidie halmashauri hizi ziweze kuzikabili changamoto na kupata nguvu na uwezo wa kutekeleza majumu yake,” alisema.

Dk. Asha-Rose alisema ingawa uwajibikaji wa jumuia za kimataifa ni muhimu katika upatikanaji wa fedha na utaalamu, bado wajibu wa serikali za mitaa katika kufanikisha malengo ya milenia unahitajika.


000000000000000000000000000

Athari za utani wa ‘mchumba’ kwa wasichana

* Mmoja apata mimba na kutelekezwa

NA JANE MIHANJI

JANDO na Unyago ni mila zilizokuwepo zamani ambazo zilikuwa zikiwafundisha vijana maadili mema na jinsi ya kuishi katika jamii.

Kwa mabinti ambao walikuwa wamebalehe hawa waliitwa na mabibi au mashangazi na kupewa mafunzo maridhawa ya maisha kwa jumla. Ikiwa ni pamoja na usafi wa mwili, upendo, uvumilivu, kujituma katika ufanyaji kazi na suala zima la heshima kwa mkubwa na mdogo.

Halikadhalika jando kwa wanaume. Hawa walipelekwa porini kwa makundi yenye umri wa rika moja huko pamoja na kutahiriwa, basi hufundishwa mambo mengi ikiwemo kuwa mioyo ya ujasiri. Tena wakati huo walikuwa wakiingizwa suna bila hata ganzi.

Siku hizi maadili hayo yanapotea, usasa unawaingiza mabinti wa kike kwenye mambo ya ajabu. Vitu kama kitchen party kwa walio wengi ni kufanya mambo ya kishangingi, kuonyesha viungo vyao na michezo ya ajabu.

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakidiriki kuwafundisha mabinti hawa kuwa ni lazima kuwa na mafiga matatu kwani moja haliwezi kuinjika chungu.

Hivi karibuni baadhi ya waandishi wa habari kutoka chama cha Waandishi wa habari za ukimwi na afya (AJAAT) walitembelea wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kukutana na baadhi ya mambo ambayo pengine yamesababisha na watoto kutoelezwa bayana madhara ya mambo fulani katika maisha.

Selina (siyo jina halisi) ni binti ambaye alipata mimba bila kujua. Akiwa na bibi yake aliweza kusimulia jinsi alivyopata ujauzito huo aliokuwa hajaupanga.

“Kuna kaka alikuwa akinitania na kuniita mchumba, utani huo uliendelea na alikuwa akinipa vitu vidogo vidogo. Wakati wa sikukuu nilimfuata na kumwomba aniletee zawadi huku nikimwuliza kama kweli atanioa.

“Akaniambia ukitaka nikuoe nipe kidogo nionje.Aliniingiza chumbani kwake na nikafanya naye tendo la ndoa. Alikuwa ni mwanaume wa kwanza na siku hiyo hiyo nilipata mimba,” anasema Selina.

Siku zilivyozidi kwenda alikuwa akijisikia homa za hapa na pale, hadi bibi yake alipokuwa kugundua kwamba ana mimba.

Selina akuwahi kwenda kliniki kuangalia afya yake na hali ile ya ujauzito. Siku moja aliamka asubuhi na kusikia amebanwa na haja. Aliingia chooni na kutaka kumaliza matatizo yake, alipojaribu kujikamua aliona hakuna kitu, aliendelea kukaa chooni na baadaye kusikia kitu kizito kikichoropoka na kusikia mlio.

Kumbe alikuwa amejifungua mtoto wa kiume, alianza kulia na kupiga mayowe, majirani walifika na kumsaidia ambapo mtoto yule aliokolewa. Yaliyomkuta Selina ni kupelekwa katika kituo cha polisi na hatimaye mahakamani kwa kujibu mashitaka ya kutaka kuua.

Wakati huo Selina alikuwa na umri wa chini ya miaka 18. Swali la kujiuliza ni kwamba nani alimfundisha Selina hatari ya tendo la kujamiiana? Nani alipata fursa ya kumweleza dalili za hatari kwa mama mjamzito, au dalili za kutaka kujifungua. Hakuna.

“Jando na Unyago ilijumuisha pia suala zima la mahusiano ya kimwili na elimu ya uzazi pia,” anasema Mustapha Selemani na kubainisha kuwa katika suala zima ya elimu ya afya ya uzazi, wazee walikuwa wakitumia zaidi mbinu za kienyeji kwa maada ya kutumia wakunga wa jadi.

Anasema ilikuwa ni jambo la kawaida wazee kuzalisha mabinti zao nyumbani na hakukua na haja ya watu kwenda hospitali, kwanza kutokana na kuwa mbali na vituo vya afya.

Selina kama mabinti wengine wengi, alikosa elimu ya afya ya uzazi. Magreth Shoo ambaye ni muuguzi anasema kuwa ni vema elimu hiyo ikawa inatolewa shuleni.

“Kuna taasisi mbalimba mbali na vyama vya kijamii siku hizi vimekuwa vikianzisha klabu katika shule mbalimbali za sekondari na kuzungumza na wanafunzi juu ya afya ya uzazi, ukimwi na mambo mengi ambayo chanzo huwa ni mahusiano kati ya wanaume na wanawake,” alisema Magreth.

Hussein Yahya, fundi viatu mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam anasema kuwa tabia ya kuzoesha watoto au kuwatania kuita mchumba ni mbaya sana na jamii ikemee.

“Wanaume watu wazima ndiyo wanatabia hii, binafsi siipendi kabisa, mchumba mchumba mwisho inaa mchumba, nimeshashuhudia matukio ya utani wa namna hiyo na baadaye kutokea kwa madhara,” anasema Yahya.

“Akina mama ambao mara nyingi ndiyo huwa na watoto, wakatae tabia hii kabisa siyo nzuri hata kidogo…kwanza mtoto unapomwita hivyo unampa mtihani wa kutaka kujua nini maana ya mchumba, kazi hapo ndiyo inapoanza akija kufahamu, mimi nikisikia mwanangu anaitwa mchumba, huyo mtu tutapambana naye kwasababu nimeshakutana na matukio ya namna hii ambayo baadaye huleta madhara,” aliongeza.

Kwa upande wake, Selina anasema aliona kama ananyanyaswa na kitendo cha kupelekwa polisi na hatimaye mahakamani. Kwani yeye ndiye alikuwa anajua ukweli kwamba hakuwa na nia ya kutaka kumwuua mtoto yule.

“Lakini namshukuru mwanasheria mmoja niliyempata kupita shirika moja la haki za binadamu Dar es Salaam ambaye alinisaidia na nikaachiwa huru. Kwani awali nilikuwa rumande na mtoto. Baadaye nikaachiwa kwa dhamana lakini baadaye kesi haikuendelea,” anasema.

Pamoja na kwamba Selina alibebeshwa mzigo huo mzito na mwanaume, katika tabu zote na misukosuko aliyoipata alijikuta yuko peke yake. Kijana yule alimaliza uhusiano na Selina baada ya kugundua tu kwaba Selina yu mjamzito.

Alimkatisha masomo yake ya elimu ya msingi. Hakuweza kuchukuliwa hatua zozote. Anasema wakati ule hamasa za kuwatia jela wanaopa mimba za wanafunzi hazikuwepo.

Analalamika jinsi maisha yake yalivyokuwa magumu na kusema kuwa asingepata mimba na kuacha shule, pengine angekuwa na maisha mazuri kidogo kuliko ya hivi sasa anayoishi bila kazi.

Selina anasema baada ya kukumbwa na mkasa huo, hapendi kuona mwanamke ananyanyasika au kupata matatizo yanayosababishwa na wanaume.


000000000000000



Watuhumiwa wa ugaidi wabambwa kwenye ndege


* Ni kwa tuhuma za kutaka kufanya ugaidi

COLOGNE, Ujerumani

MAKOMANDO wa Ujerumani wamewakamata watu wawili waliokuwa wanasakwa kwa tuhuma za ugaidi, katika ndege ya KLM iliyokuwa ikijiandaa kuruka kutoka jijini hapa.

Kwa mujibu wa Polisi, watu hao wawili, raia wa Somalia na mwingine msomali aliyezaliwa Ujerumani, inadaiwa walikuwa wakijiandaa kufanya mashambulizi, na wamekamatwa baada ya kufuatiliwa kwa miezi kadhaa.

Ofisa wa Polisi aliieleza televisheni ya hapa, kuwa watu hao walikuwa wakijiandaa kuendesha 'vita vitakatifu', na kwamba taarifa za mipango hiyo zilikutwa nyumbani kwao.

Ndege hiyo ya KLM ilikuwa ikijiandaa kwenda Amsterdam, Uholanzi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi,Frank Scheulen, alisema makomando walipanda kwenye ndege hiyo ilipokuwa inakaribia kuruka na kuwakamata watu hao.

Baadaye abiria wote waliamriwa kushuka kwenye ndege hiyo kwa ajili ya kukagua mizigo, kabla ya kuruhusiwa kuruka saa moja baadaye.Ndege hiyo ilitua salama Amsterdam.


00000000000

Kuna mchanga unaohama Ngorongoro


AMA kweli kutembea ni kuona mengi, ndivyo tunavyoweza kusema. Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vya utalii ambavyo wengi wetu hatuvijui.

Katika Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro (NCAA) iliyoko mkoani Arusha kuna mchanga unaohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa wastani mita 100 kila mwaka.

Mchanga huo umejikusanya mithili ya kichuguu, na ‘husafiri’ kutoka mahali unapokuwa kwenda mashariki mwa hifadhi hiyo.

Kwa sasa, mchanga huo uliopewa jina la kiingereza la ‘moving sand’ uko takribani kilometa 40 kutoka mahali yalipo makumbusho ya Oldupai (Olduvai) ndani ya hifadhi hiyo.

Pamoja na maajabu hayo ambayo yalibainishwa na watafiti wa mambo ya kale waliokuwa wakifuatilia jinsi binadamu wa kale alivyoishi, waligundua pia kwamba huwa hauchani.

Badala yake, husafiri jinsi ulivyo bila kuacha chembe nyuma. Kwa miaka mingi umekuwa kivutio kikubwa cha watalii wanaotembelea eneo la hifadhi.

Watafiti wanasema, aina hiyo ya mchanga hupatikana karibu na ziwa Manyara, lililoko nje kidogo ya hifadhi hiyo.

Wamasai ambao ni miongoni mwa makabila yanayoishi ndani ya hifadhi hiyo huutumia kutoa kafara na kufanya matambiko mbalimbali.

Matambiko hayo hufanywa ili wapate ‘baraka’ kutoka kwa Mungu na pia kuzaa watoto wengi kwa jinsi wanavyopenda. Ili kufanikisha matakwa yao, huchinja wanyama tofauti kama sehemu ya tambiko.


000000000000

Maradhi ya upotevu wa kumbukumbu


BAADHI ya watu wanapofikia umri wa uzeeni hukabiliwa na maradhi ya kupungua uwezo wa kuweka kumbukumbu na hata kuchanganua mambo.

Mazingira ya namna hiyo huweza kuwapata pia baadhi ya watu, bila kujali kuwa wamefikia katika umri huo wa uzee.

Wakati mwingine, mtu mwenye maradhi ya namna hiyo, waweza kudhani ni mwehu, kwa sababu kwa sababu wakati unazungumza naye, anaweza kutamka ghafla jambo ambalo ni kinyume kabisa ama halihusiani na mada mnayozungumzia.

Kwa maneno mengine ya mitaani, vijana husema kuwa mtu wa namna hiyo anapoteza ‘network’.

Haya ni maradhi ambayo yamekuwa yakiwasumbua wengi japokuwa pale yanapotokea kwa wazee, huyachukulia tu ni hali ya uzee.

Wanasayansi wanasema kuwa inapokuwa siyo uzee basi maradhi hayo yanaweza kuoanishwa na ajali ambayo mtu aliipata katika historia ya maisha yake.

Wanasayansi wanasema haya siyo maradhi ambayo mtu anazaliwa nayo bali humtokea akiwa tayari ameanza kuishi.

Kwa kawaida tatizo hilo huanza kwa mtu polepole kupoteza kumbukumbu ikifuatiwa na mtu kushindwa kufanya kazi ambazo kawaida zilikuwa ndani ya uwezo weke.

Hatua inayofuatia anakuwa anachanganya mambo, mathalan ulikuwa umeshinda naye siku nzima anakuuliza, umerudi saa ngapi?
Wewe utashangaa kwanini akuulize hivyo wakati wote mlikuwa pamoja.

Mtu wa namna hiyo pia akienda mahali huweza kusahau njia ya kurudi nyumbani japokuwa inawezekana kabisa alizaliwa na kukulia mazingira yao.

Katika hatua nyingine atapoteza kabisa mawasiliano na hata uwezo wa kujitambua kiasi kwamba hata kama yu uchi hatakuwa na ufahamu wa kujisetiri. Maradhi haya ni tofauti na wehu au utimbio wa ubongo.

Lakini, wanasayansi wanaamini pia kuwa maradhi haya huweza kuwa na uhusiano wa athari za ajali iliyompata mtu muda mrefu ama miaka kadhaa.

Kama kawaida, wanasayansi wapo kwenye tafiti mbalimbali juu ya madhara hayo na hivi karibuni wamekuja na jipya.

Hili ni kundi la wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Tiba Washington, Marekani pamoja na Chuo Kikuu cha Tiba Milan, Italia wameweza kutambua jinsi maradhi haya yanavyotokea.

Baada ya pekenyupekenyu zao walibaini kuwa hali hiyo inatokana na mabadiliko ya aina fulani ya protini kwenye ubongo inayojulikana kama amyloid beta.

Wao walibaini kuwa uzalishaji wa aina hii ya protini unapopungua unaongeza uwezekano wa kupatwa na maradhi hayo na inapozaliswa kwa kiwango kinachotakiwa, basi uwezo wa mawasiliano unakuwa katika hali nzuri.

Katika kuendesha utafiti huo, walichukua umajimaji uliopo katikati ya seli za ubongo kwa mtu mgonjwa ambaye alikuwa katika hali mbaya ambayo inahitaji kuwa na usaidizi wa karibu wa madaktari.

Majaribio hayo waliyafanya kwa watu 18 tofauti ambao ndugu zao walitoa ruhusa kwa madaktari hao kufanya hivyo kwa malengo ya utafiti.

Ndipo wakabaini uwepo wa aina hii ya protini lakini, ikabidi wajaribu kuona ni kitu gani kinachochochea kupungua amyloid beta wakati mtu akipata ajali hasa zinazohusiana na maeneo ya kichwa.

Kwa maneno mengine ni kwamba walijaribu kuchunguza kitu kinachosababisha mtu apate ajali, halafu awe amepona kabisa na kuendelea na shughuli zake lakini baadae ghafla maradhi haya yamkumbe.

Profesa David L. Brody wa Chuo Kikuu cha Washington ambaye alikuwa mmoja wa waandamizi kwenye utafiti huo, alisema kuwa kwa kawaida mgonjwa anakuwa tayari na maradhi hayo kabla hajapata ajali.

“Ajali inakuwa tu ni jambo ambalo linaharakisha dalili za ugonjwa huu na siyo kwamba yenyewe ndiyo inasababisha,” alisema Profesa Brody.

Lakini, anasema kuwa bado hawajajiridhisha katika utafiti huu kwa sababu bado kuna mambo ambayo wanapaswa kuyang’amua.

Hii ni pamoja na sababu zinazosababisha ajali kuchochea maradhi hayo na kwa maana kwamba kuathiri uzalishaji wa amyloid beta.

Utafiti wa wanasayansi hao unalenga zaidi katika kuweza kupata dawa muafaka kwa ajili ya kutibu maradhi haya.

Kwa sasa hakina tiba ya moja kwa moja bali madaktari hujaribu kupunguza athari zinazoandamana na maradhi.

Mara nyingi, tiba hii huwa na mafanikio mazuri kwenye hatua za mwanzo za maradhi hivyo tafiti za wanasayansi hawa huenda zikaja na uwezo wa kuzuia na hata kutibu kwa uhakika kwa wale ambao tayari wameathirika.


00000000000000

Utajisikiaje ukigundua gari unalotanua nalo mkeo alihongwa?


WASOMAJI wangu karibuni tena katika safu muipendayo ya Pasua Kichwa, wiki hii nina kitu kingine cha kupasua bongo zenu kisawa sawa.
Kuna jamaa mmoja alikuwa anaishi mitaa ya Ilala, mshikaji tulikuwa tunamuita baharia kwa sababu alifanya sana kazi hiyo zamani katika nchi mbalimbali za Ulaya.
Labda ndugu au jamaa zake wa karibu tu ndio walijua sababu ya kwanini, Baharia alirudi Tanzania na kuendesha maisha kupitia biashara ya nguo na vipodozi.
Jamaa alikuwa na roho nzuri kwa majirani zake na katika kushirikiana kwake na watu mbalimbali, ndipo siku moja akajikuta anamtongoza msichana mmoja wa maeneo ya Kinondoni.
Msichana huyo alikuwa anafanya kazi hoteli moja ya kifahari katika jiji la Dar es Salaam na huenda alikuwa miongoni mwa wakubwa kutokana na gari ya ofisi kumfuata na kumrudisha.
Baharia na msichana huyo wakawa hawakauki machoni mwetu pale mitaa ya Ilala.Wambeya na wakware wa ngono walimmezea mate sana msichana huyo kutokana na kuwa na umbo la kuvutia.
Siwezi kukwambia umbile lake lilivyo ila mitaani baadhi ya vijana hupenda kuwaita wanawake wa kuchora. Yaani paja paja kwelikweli, guu usiseme,kihuno namba nane, shingo kama ya twiga. Nadhani wengi mtakuwa mmeona michoro ya wanawake wa aina hiyo kwenye majarida ya kibongo.
Msichana huyo baada ya kuzama kwenye penzi la Baharia karibu mwaka mmoja, hatimaye wakafunga ndoa.
Kila mmoja alibaki na shughuli zake na mara mwanamke akaanza kubadilisha magari kama njugu. Mara kaja na Toyota Cresta, Sprinter, Suzuki, Prado, Benzi na mengine tele.
Binadamu hakosi wivu. Ghafla Baharia akaanza kuwa mbogo kwa mkewe na hata kufikia kumdunda hadi kumtoa manundu pale alipojibiwa vibaya au kutoridhishwa na majibu ya mkewe.
Jamaa alikuwa anamuuliza mke wake magari hayo ya nani mwanamke anasema yapo aliyonunua kwa fedha zake na aliyopewa na wazazi wake na mengine ya ofisini kwao.
Akiomba nyaraka ili kuthibitisha umiliki hapewi na mwishowe wanaishia kugombana na kupata suluhu wenyewe.
Baharia alikuwa mkali wee mwishowe akalainika kwa kuzingatia alikuwa anaumia roho sana kila alipokuwa anaambiwa atoe talaka kama anaona hayo magari yanamtia wazimu.
Basi akajikuta naye anaendesha moja kati ya magari hayo na siku hiyo Baharia akiwa mitaa ya Magomeni alisimamishwa na jamaa mmoja.
Mwenyewe alijua ni miongoni mwa watu anaojihusisha nao kibiashara,ile kushuka tu kwenye gari akaambiwa kwa sauti kali atoe funguo kabla hajakwenda kulala jela.
Baharia akagoma na kumwambia jamaa ni jambazi, kauli hiyo iliamsha hasira za huyo jamaa na kuanza kumsemea mbovu mwanaume mwenzake.
"Wee nini, hili ni gari langu kama mwanamke wako amekwambia lake kakuficha, leta funguo zangu siwezi kuhonga mwanaume mwenzangu," jamaa alimbwatia Baharia.
Zogo likajaza watu hadi polisi wakafika na kuamua kuwapeleka wahusika kituoni ambako jamaa alikabidhiwa gari lake baada ya kuonyesha nyaraka mbalimbali.
Baharia akawekwa selo ili kutoa maelezo polisi alilipataje, ndugu zake ndio walikwenda kumwekea dhamana akatoka na kurudi nyumbani kwake Ilala kwa daladala, je kama ingekuwa wewe ungefanyaje? tuma katika namba 0777 167514.


00000000

No comments: