Saturday, October 4, 2008

vijimambo vya ndani ya nchi

Watoto waliokufa Tabora watajwa


* Rais Kikwete, CCM watuma rambirambi
* NSSF yatoa ubani 500,000/- kwa kila familia

Na El - hadji Yuusuf, Tabora

MAJINA ya watoto 19 waliokufa kwa kukosa hewa katika ukumbi wa disko mjini hapa, wakati wa kusherehekea sikukuu ya Idd el-Fitri juzi, yametajwa.

Wakati majina hayo yakitajwa, Rais Jakaya Kikwete, ametuma rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na wazazi wa watoto hao.

Watoto hao walianguka baada ya ukumbi wa Bubbles Night Club na Oneten Disko Teck, katika maghorofa ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kutokuwa na hewa ya kutosha, hivyo kusababisha vifo na wengine kujeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa, alisema tukio hilo limeshitua wengi na kwamba limeleta hali ya fadhaa kwa wazazi na walezi.

Aliwataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa Veronica Maningu, Beatrice Makelele, Jacob Gerald, Salma Hamis, Hadija Waziri, Rehema Moyo, Seleman Idd, Mrisho Seleman, Abdallah Rehani na Agatha Maningu.

Wengine waliopoteza maisha ni Paulina Emmanuel, Ramla Yenga, Mohamed Kapaya, Habiba Shaaban, Donald Kasela, Mwanahamisi Waziri, Philipo Haule, Ashura Jamal na Yassin Rashid.

Mwinyimsa aliwataja watoto waliozimia na kulazwa katika hospitali ya mkoa wa Tabora ya Kitete kwa matibabu kuwa, Sakina Ali, Daudi Chape, Shufaa Azan, Naomi Joseph, Amani Emilian, Jumanne Mashaka, Kulwa Iddi, Msimu Rehani, Bahati Hamisi na Bertha Maneno.

Wengine waliolazwa ni Asia Mohamed, Mwami Masumbuko, Shida Kassim, Kenea Masudi, Agness Kasele, Josephine Julius, Tatu Hamad na Ramadhani Idd.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tabora, Daudi Siasa alisema watoto 10 waliruhusiwa kutoka hospitalini jana, huku sita wakiendelea na matibabu.

Kutokana na tukio hilo, Mwinyimsa alisema serikali kupitia vyombo vya usalama, imeanza kuchukua hatua madhubuti baada ya kuwakamata watu waliokuwa wakipiga disko katika kumbi za Bubbles na Oneten katika jengo la NSSF yalikotokea maafa hayo.

Mbali na kukamatwa kwa watu hao, alisema serikali imeunda tume itakayofanya kazi kwa siku saba kuchunguza chanzo cha tatizo hilo.

Alisema tume hiyo itahusisha watu kutoka idara za ujenzi, Jeshi la Polisi na usalama wa taifa na inatakiwa kuwasilisha taarifa wiki ijayo.

Mwinyimsa alisema serikali itagharamia maziko ya watoto hao, na kutoa ubani wa sh. 50,000 kwa kila mzazi, ikiwa ni pamoja na kupendekeza watoto hao wazikwe mahali pamoja kwa ajili ya kuweka kumbukumbu rasmi.

Kwa mujibu wa watoto walionusurika katika ajali hiyo ndani ya kumbi hizo za starehe zilizo katika eneo moja, kulikuwa na joto kali na kulikuwa na harufu mbaya.

Walisema hali hiyo ilisababisha takriban watoto 50 kuanguka, ambapo 19 walikufa.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ametuma rambirambi na kutuma ujumbe maalumu utakaoongoza shughuli za maziko zinazotarajiwa kufanyika mjini Tabora.

Ujumbe huo utaoongozwa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya.

Rais alisema amepokea kwa mshituko mkubwa habari za vifo vya watoto hao na amehuzunishwa na kusikitishwa na msiba huo.

“Nimepokea kwa mshituko mkubwa, huzuni nyingi na masikitiko yasiyokuwa na kifani habari za vifo vya watoto hao wasiokuwa na hatia, ambao walikuwa wanasherehekea sikukuu ya Idd el Fitri kama tulivyokuwa tunafanya sisi sote,” alisema Rais.

Aliongeza: “Mawazo yangu yote yako kwa wazazi na wanafamilia wa watoto hao katika kipindi hiki kigumu cha huzuni, majonzi na msiba mkubwa. Tunawaombea kwa Mwenyeji Mungu waweze kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu”.

Rais Kikwete alisema ni matarajio yake kuwa, vyombo vya sheria vitachunguza kikamilifu na ipasavyo vifo vya watoto hao na kuchukua hatua zinazostahili.

Kwa upande wake, Profesa Kapuya akitoa salamu za Rais, aliuambia umati uliokusanyika katika hospitali ya Kitete mjini Tabora kwa ajili ya kuchukua miili ya marehemu hao, kuwa NSSF itatoa ubani wa sh. 500,000 kwa kila familia iliyopoteza mtoto.

Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa rambirambi kutokana na vifo hivyo.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Halamshauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, John Chiligati, ilisema Chama kinaungana na serikali na wazazi wa watoto waliopoteza maisha katika kipindi hiki kigumu.

Chiligati alisema ni vyema wananchi, hususan wazazi wa watoto hao kuwa na subira wakati huu, ambapo tume iliyoundwa inachunguza chanzo cha tatizo hilo


00000000000000

• Ni simanzi tu Tabora


* Baadhi ya watoto wazikwa
* Karume atuma rambirambi

Na El - hadji Yuusuf, Tabora
WAZIRI wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, jana aliwaongoza mamia ya wakazi wa Tabora, katika mazishi ya watoto 19 waliokufa kwa kukosa hewa wakiwa kwenye kumbi za disko kusherehekea sikukuu ya Idd el Fitri.

Mazishi ya watoto hao yalifanyika kwenye maeneo mbalimbali, Profesa Kapuya, ambaye alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete, alihudhuria ya watoto wanne.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi ya watoto hao ni Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki, mkoani humu na mkewe, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margaret Sitta, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu.

Wengine ni Mkuu wa mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau. Maafa hayo yalitokea kwenye jengo la shirika hilo.

Profesa Kapuya, ambaye ni Mbunge wa Urambo Magharibi, alihudhuria mazishi ya watoto hao, waliozikwa katika maeneo ya Ng’ambo na Rufita.

Spika Sitta alihudhuria kwenye mazishi ya watoto wawili yaliyofanyika eneo jirani na uwanja Ali Hassan Mwinyi.

Watoto hao walikubwa na maafa hayo Jumatano wiki hii, wakiwa disko kwenye kumbi za Bubbles Night Club na Oneten Disco Theque.

Watoto 16 walijeruhiwa, ambapo hadi jana wanne bado walikuwa wakiendelea na matibabu kwenye hospitali ya mkoa ya Kitete.

Kwa mujibu wa Mwinyimsa, hali za watoto hao zinaendelea vizuri, licha ya kukaa muda mrefu bila ya kupata fahamu.

Aliwashukuru wananchi kwa kuwa watulivu tangu mkasa huo ulipotokea na kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi hiki kigumu.

Akizungumzia kuhusu tume aliyoiunda kuchunguza tukio hilo, alisema inaanza kazi leo.

Alisema moja ya mambo ambayo yanatarajiwa kupatiwa ufumbuzi na tume hiyo ni kujua kama wafanyabiashara wa kumbi hizo walifuata sheria na taratibu, kama kumbi hizo zilikuwa na nafasi ya kutosha na vifaa vya tahadhari.

Mwinyimsa alisema tume hiyo itawahoji watu muhimu na wale ambao wataonekana kuwa na uwezo wa kutambua kilichojiri katika ukumbi huo, wakiwemo watoto walionusurika.

Aliwataja watu wengine ambao tume hiyo inatarajiwa kuwahoji kuwa, wamiliki wa kumbi hizo, mameneja, wazuia fujo katika kumbi hizo na watu wengine watakaojitokeza, ambao wanaweza kuipa ushirikiano tume kufanyakazi vizuri.

Mwinyimsa alisema polisi inawashikilia Shashikant Patel, mkurugenzi wa Bubbles Night Club na meneja wake Vituko Salala.

Wengine ni Mkurugenzi wa Oneten Disco Theque, Projestus Fidelis ‘Porojo’ na meneja wake, Jaffar Rashid.

Alisema walinzi wa milangoni waliokimbia baada ya tukio hilo, wanaendelea kusakwa na polisi.

Kwa mujibu wa Mwinyimsa, serikali itachukua hatua dhidi ya watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kusababisha tukio hilo.

Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, ametuma rambirambi kwa wananchi wa Tabora kutokana na vifo hivyo.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Rais Karume alieleza kushtushwa na vifo hivyo, vilivyohusisha watoto wadogo wasio na hatia.

Alisema taifa limepata hasara kuwapoteza watoto, ambao ni matumaini ya wazazi na taifa.

Katika hatua nyingine, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, imetuma rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watoto waliofariki dunia katika tukio hilo.

Rambirambi hizo zilitolewa jana na wizara kupitia Msemaji wake Erasto Ching'oro, aliyesema wizara imepokea kwa masikitiko makubwa na kwamba msiba huo ni wa taifa.

Wakati huo huo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimetoa pole kwa familia za watoto hao, na kuitaka serikali ichukue hatua kuhakikisha viwanja vya michezo na burudani vilivyoporwa na matajiri vinarejeshwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Ananilea Nkya, alisema wamekuwa wakifuatilia na kubaini katika miaka ya hivi karibuni maeneo mengi yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya michezo yamegeuzwa viwanda vidogo, gereji, baa, migahawa, maduka, hoteli na vituo vya mafuta.


000000000000000

• Uchunguzi makini ufanyike vifo vya watoto Tabora


MAONI……

MARA kwa mara, wakati wa maadhimisho ya sikukuu, limekuwa jambo la kawaida kuripotiwa watu kufa katika ajali za barabarani na wengine kupigwa kutokana na ugomvi, hususan kwenye maeneo ya starehe.

Katika maadhimisho ya sikukuu ya Idd el-Fitri yaliyofikia kilele juzi, pia kumeripotiwa kutokea mambo mbalimbali katika sehemu mbalimbali hapa nchini yakiwemo ya watu kupoteza maisha.

Licha ya kuwepo mambo mengi, kubwa zaidi ni la kupoteza maisha kwa watoto 19 kwenye ukumbi wa disko huko Tabora. Hayo ni maafa makubwa na ya kutisha.

Imeripotiwa kuwa watoto hao, wanane wakiwa wavulana na 11 wasichana, walikufa kutokana na kukosa hewa katika ukumbi wa disko wa Bubbles,na oneten,zilizoko katika jengo linalomilikiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa, watoto waliokufa wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka saba na 18. Wengine 16 walilazwa katika hospitali ya mkoa, watatu hali zao zikiwa mbaya.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watoto hao walijaa kupita uwezo wa ukumbi, jambo lililosababisha mzunguko wa hewa kuwa mdogo.

Wakurugenzi kadhaa wa ukumbi huo imeelezwa wanashikiliwa na polisi kwa kuhojiwa kuhusu tukio hilo la kusikitisha.

Mwinyimsa alisema kamati imeundwa kuchunguza tukio hilo, ikihusisha maofisa kutoka Polisi, Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Tukio hilo linaonyesha wazi kwamba, wenye ukumbi hawakuwa makini katika kusimamia shughuli hiyo.

Ni jambo lililo dhahiri kwamba walijali zaidi maslahi binafsi, badala ya afya za walioingia kwenye ukumbi huo.

Katika msongamano huo, licha ya waliopoteza maisha, kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya watoto hao kuambukizwa maradhi yanayoenezwa kwa njia ya hewa.

Wakati tunaungana na familia za watoto waliopoteza maisha, tungependa kushauri mambo kadhaa juu ya hatua ambazo tunadhani zinafaa kuchukuliwa.

Kwanza, tume iliyoundwa kuchunguza maafa hayo ifanye kazi kikamilifu na umakini mkubwa, ili matokeo yatoe picha halisi ya chanzo chake.

Pili, kwa kuwa uchunguzi unahusisha vyombo vya dola basi endapo itabainika kuwepo uzembe kwa upande wowote hatua stahiki zichukuliwe kwa waliohusika.

Tunasema haya kwa sababu hatuamini kwamba watoto wanaweza kujaa kwenye ukumbi kiasi cha kukosa hewa bila tahadhari yoyote ya madhara ambayo yangeweza kutokea.

Hivyo katika uchunguzi huo, ni vyema jengo hilo likachunguzwa ujenzi wake, na ikibainika haukuzingatia taratibu na halifai kwa shughuli za disco wahusika wawajibishwe.

Kwa kifupi mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kwa wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo, ili lisijirudie katika siku zijazo.


00000000000000000

Mgombea ugavana amtwanga mwandishi


BANGKOK, Thailand

MMOJA wa wagombea ugavana wa jiji la Bangkok juzi alimshambulia kwa ngumi na mateke mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni kwa madai ya kukerwa na maswali magumu.

Mgombea ugavana huyo, Chuvit Kamolvisit alikuwa akiulizwa na mwandishi huyo, huku mahojiano hayo yakirushwa moja kwa moja.
Hata hivyo, mgombea huyo aliomba radhi, akisema alipandwa na ghadhabu baada ya kuona kuwa maswali ya mwandishi huyo, Visam Dilokwanich, yanalenga kumuumbua ili anyimwe kura kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika kesho.

“Nakiri nilifanya hivyo. Sikuvumilia kwa kuona ananiumbua moja kwa moja kupitia televisheni,” alisema Chuvit, mtu wa miraba minne aliyewahi kumiliki baa kadhaa jijini Bangkok, zenye wahudumu wanaovalia vivazi vya nusu uchi.

“Nilichofanya ni uhalifu, na ni haki kwangu kulipa faini kwa kumdunda kwa ngumi na mateke,” aliongeza Chuvit, ambaye hana nafasi kubwa ya kushinda kwenye uchaguzi huo.
Mwanahabari huyo alifungua kesi polisi, akisema Chuviot alionekana kama jambazi.

“Alikasirika sana nilipomwambia kwamba alichokuwa akisema katika mahojiano hayo yalikuwa tofauti sana na anachokisema akiwa sehemu nyingine,” alieleza Visarn, akiwaonyesha wanahabari wenzake majeraha aliyopata shingoni na kichwani baada ya kipigo.


00000000000000

• Ndege tano zaporwa Mexico


MEXICO CITY, Mexico

WATU wenye silaha juzi walipora ndege tano ndogo kutoka kwenye uwanja binafsi, katika mji wa Kaskazini Magharibi mwa Mexico wa Sinaloa, baada ya kumzidi nguvu polisi.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, waporaji hao, wanaokadiriwa kufikia 20, walivamia uwanja huo mdogo wa ndege alfajiri, wakamnyang’anya polisi bunduki, wakamfunga kamba, wakajaza mafuta katika ndege hizo, na hatimaye wakaruka.

Msemaji wa kikosi cha polisi kinachopambana na mtandao wa kihalifu, Emma Quiroz alisema kuwa haikufahamika iwapo kuna uhusiano kati ya waporaji hao na genge linalojihusisha na dawa za kulevya aina ya ‘cocaine’.

Kundi hilo kwa kawaida hutumia ndege ndogo kusafirisha dawa hizo Kaskazini mwa Mexico hadi mpakani na Marekani.
Alieleza kuwa polisi wanachunguza iwapo uporaji huo ulifanikishwa kwa msaada wa baadhi ya maofisa serikalini.

Taarifa ilieleza kuwa vyombo vya usalama vilikuwa vikifuatilia kujua wapi ndege hizo zimepelekwa, na pia kuwakamata waporaji. Alisema ziliporwa eneo la kufanyia matengenezo kwenye uwanja huo unaomilikiwa na kampuni ya kunyunyizia dawa mazao ya kilimo mjini Navolato.

Jeshi lilizisimamisha ndeghe hizo kutoa huduma mapema mwaka huu, kwa maelezo kuwa hazikuwa katika hali nzuri ya kukidhi usalama wa anga.

Jeshi la ulinzi, ambalo pia linashiriki kukabiliana na genge la dawa za kulevya nchini Mexico, na hasa kwenye majimbo ya Kaskazini, limeshakamata ndege ndogo 245, zikiwemo helikopta, tangu Novemba, mwaka jana.

Sinaloa ni moja ya majimbo ambako magenge yanayojihusisha na biashara ya dawa za kulevya yanakabiliana vikali na jeshi, ambalo kwa mwaka huu pekee limeua watu wapatao 3,000. Ndege ndogo hutumiwa kihalali kunyunyizia dawa mazao mashambani, na vilevile kuteketeza kilimo cha bangi.


00000000000000

No comments: